Kwa masikitiko makubwa, Bodi ya Udhamini wa Mfuko wa Wanawake Tanzania, Women Fund Tanzania Trust (WFT Trust), Uongozi, Wafanyakazi, na kwa niaba ya wanamtandao wenzetu, tunatoa taarifa ya msiba wa aliyekuwa Mjumbe wa Bodi ya Wadhamini wa Mfuko na Mwenyekiti wa kamati ya kiufundi ya utoaji ruzuku na mwanaharakati mwenzetu mpendwa dada yetu, Christina Warioba aliyefikwa na mauti siku ya Jumatatu,Mei 30, 2022.
Dada Christina alikuwa mtaalamu na mtetezi mbobezi wa haki za wanawake, usawa wa kijinsia, na maendeleo ya kijamii. Tunaposherehekea maisha ya mpendwa wetu Dada Christina tunaenzi na kutambua alivyokuwa akijituma na kujitolea kwa kiwango kisichopimika ili kuendeleza harakati za usawa wa kijinsia nchini Tanzania na kwingineko.
Women Fund Tanzania Trust inatambua, inashukuru na kuenzi juhudi zake katika kuimarisha uwezo wa kitaasisi katika kipindi chote cha uhai wake. Daima tutaenzi mchango wake mkubwa kwenye upanuzi wa programu za WFT Trust katika kutoa ruzuku zilizoweza kuwafikia wanawake na wasichana wengi wenye uhitaji katika maeneo mbalimbali na hasa pembezoni mwa nchi yetu.
Tunachukua fursa hii kuungana na wanaharakati watetezi wa haki za wanawake hapa Tanzania na nchi za kanda ya Kusini mwa Afrika (SADC) kuenzi, kutambua, na kuthamini mchango wa mpendwa wetu Dada Christina katika kuchagiza utekelezaji wa mikataba ya kimataifa na kikanda inayohusu haki za wanawake na usawa wa kijinsia ikiwemo Azimio la Beijing na lile la usawa wa kijinsia katika kanda ya Kusini mwa Afrika (SADC). Dada Christina atakumbukwa kwa kuendeleza jitihada za uzingatiaji wa misingi ya usawa wa kijinsia na haki za wanawake katika sera, michakato ya maendeleo, pamoja na kujenga uwezo wa taasisi na makundi mbalimbali na pia katika kuhimiza utekelezaji na ufuatiliaji wa matokeo. Dada Christina alitoa mchango mkubwa katika kuboresha tafiti zenye mlengo wa kijinsia ili kuwezesha utungaji wa sera na mipango iliyojikita kwenye takwimu sahihi na ushahidi wa hali halisi ya haki za wanawake na usawa wa kijinsia katika maeneo mbalimbali. Pia, Dada Christina alishiriki na kutoa mchango mkubwa katika utetezi na ushawishi katika ngazi za kisera na maamuzi ikiwemo uratibu wa awali wa jukwaa la kisera kuhusu usawa wa kijinsia na haki za wanawake ikiwemo michakato ya kujenga bajeti zenye mlengo wa kijinsia akiwa TGNP-Mtandao.
Tunapoungana na familia yake kuomboleza kifo cha mpendwa wetu Dada Christina pamoja na kuazimisha safari ya maisha yake tutaendelea kuenzi na kukumbuka uongozi wake thabiti, ubunifu, na uwezo wake mkubwa wa kujenga mahusiano na watu mbalimbali, kufuatilia fursa zinazojitokeza ili kuendeleza utetezi wa haki za wanawake na usawa wa kijinsia nchini Tanzania na kwengineko.
Daima tutakumbuka tabasamu lake mwanana, moyo wa kujitolea,msimamo thabiti juu ya haki za Wanawake na furaha iliyojaa ari, na utu wake wa kipekee.
Roho yake ya upendo na ucheshi utaendelea kuwa chanzo cha nguvu na matumaini yetu siku zote.
Umevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo umeumaliza, Imani umeilinda