UCHAMBUZI WA HOTUBA YA MHE. RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA BUNGENI KWA MTIZAMO WA KIJINSIA
APRILI 24, 2021
Mtandao wa Wanawake, Katiba, Uongozi na Uchaguzi, kwa kushirikiana na wadau wengine wanaoshughulika na masuala ya usawa wa jinsia na haki za wanawake, tunayo furaha kubwa kuendelea kumpongeza Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ameandika kestoria katika nchi yetu na ukanda wa Afrika Mashariki kwa kuwa Rais wa kwanza mwanamke Tanzania. Halikadhalika, tunampongeza Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa ujasiri wake wa kupokea Serikali na kuongoza taifa katika kipindi kigumu cha majonzi baada ya kifo cha Rais wa Awamu ya Tano Hayati Dkt. John Pombe Magufuli. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amin.
Sisi, Wanamtandao tunaoshugulika kutetea na kukuza uongozi uliojengeka katika misingi ya haki na usawa wa jinsia, tumemfuatilia kwa karibu Mheshimiwa Rais akilihutubia Bunge kwa mara ya kwanza tangu aapishwe tarehe 19 Machi 2021 na kutoa mwelekeo wa Serikali ya Awamu ya Sita kwa kipindi cha miaka mitano ijayo. Hotuba hii imeonesha vipaumbele ambavyo vimegusa maeneo mbalimbali ya maendeleo katika nchi yetu, yakiwemo yale ya kuneemesha maisha, haki, na usawa katika makundi mbalimbali ya kijamii. Kipekee tumefurahishwa na Mheshimiwa Rais Samia kwa kuonesha bayana tunu za kuongoza taifa ambazo zimejumuisha masuala ya haki, demokrasia, na usawa. Ni matumaini yetu kuwa tunu hizi muhimu zikidumishwa, kulindwa na kutetewa, zitatoa mwanga mkubwa katika kuongoza utekelezaji wa vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya sita, ambavyo vimejumuisha kukuza uchumi na kupambana na umasikini nchini, kupambana na rushwa na ubaridhifu wa mali ya umma, ulipaji wa kodi usio na bughudha, kukuza na kuongeza tija katika sekta ya kilimo na mifugo, kukuza ajira na mapato kwa kukuza na kulinda sekta ya madini, utalii, viwanda na kwingineko, kuendeleza na kukuza miundo mbinu mbalimbali, kuboresha na kuleta mapinduzi zaidi ya teknolojia, TEHAMA na mawasiliano, kuongezea uwekezaji katika sekta za nishati, elimu, afya (na haswa afya ya uzazi), kukuza na kudumisha misingi ya demokrasia, amani na uhuru, na zaidi kuhakikisha misingi ya haki na sheria zinatumika kulinda wananchi.
Tunapenda kusisitiza kuwa, katika uchambuzi wetu kuhusu Hotuba hii ya kwanza ya Mhe. Rais Samia, unaonesha kuwa maeneo yote yaliyopewa kipaumbele katika Serikali yake, yanatoa fursa kubwa ya kukuza maendeleo yatakayowafikia na kuwanufaisha wanawake, wasichana na makundi mengi mengi ya wanyonge nchini, kama utekelezaji wa vipaumbele hivi utajengeka na kutekelezeka katika misingi ya haki na usawa, ukiwemo usawa wa jinsia.
Kwa kutumia mifano michache tu hapo chini, tunaonesha jinsi maeneo yaliyobainishwa na Mheshimiwa Rais yanavyotoa fursa za kukuza misingi na matokeo ya maendeleo yatakayopelekea kukua kwa misingi inayojumuisha usawa wa jinsia, na kwa uhakika Mhe. Samia Suluhu Hassan anastahili pongezi kwa hayo:
Sisi wanamtandao tunaahidi kuendelea kufanya kazi na Serikali ya Awamu ya Sita kwa njia mbalimbali ikiwemo kutoa ushirikiano kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Awamu ya Sita katika kufuatilia na kutoa ushauri juu ya utekelezaji wa vipaumbele vilivyoainishwa katika hotuba ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan.
Imetolewa na
Mtandao wa Wanawake, Katiba, Uongozi, na Uchaguzi.
APRILI 24, 2021
Mtandao wa Wanawake, Katiba, Uongozi, na Uchaguzi unajumuisha mashirika mbalimbali, mitandao, na vikundi vya kijamii zaidi ya 150, pamoja na wanaharakati binafsi yanayojishughulisha na utetezi wa usawa wa jinsia, haki za wanawake, vijana, na watoto nchini katika sekta mbalimbali zikiwemo afya, elimu, sheria, habari, mazingira, nishati na mengineyo.